Miamba ya Ulaya Paris Saint-Germain na Barcelona zitakwaana leo usiku mechi ya kwanza katika hatua ya 16 bora Ligi ya Mabingwa Ulaya
Barcelona wameshinda mechi zao sita na kumaliza vinara wa Kundi C, ambalo pia walikuwemo Manchester City. Lionel Messi wa Barcelona kwa sasa ndiye kinara wa mabao akiwa na magoli 10 tayari kwenye kampeni hizi.
Kikosi cha Unai Emery kipo katika kiwango kizuri, wakiwa wameshinda mechi nne mfululizo. Miamba hao wa Paris hawajafungwa katika mwendo wa mechi 11 kwenye michuano yote.
Edinson Cavani amekuwa muhimili mkubwa kwa mafanikio ya PSG. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay amefunga magoli 33 msimu huu, ikiwa ni pamoja na 6 ya Ligi ya Mabingwa.
Kama ilivyo kwa wapinzani wao, Barcelona pia hawajafungwa katika mwendo wa mechi 11. Kikosi cha Luis Enrique kilishinda 6-0 mechi ya wikiendi dhidi ya Alaves kwenye Ligi ya Hispania.
Timu hizo zimekutana mara nne katika kampeni za 2014/15. mara mbili kwenye hatua ya makundi na tena kwenyo hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, ambako Barcelona walisonga kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-1.
PSG walipoteza mechi tatu katika hizo lakini walipata ushindi wa 3-2 katika Parc des Princes kwenye Kundi F.
Habari za Vikosi na Majeruhi
Thiago Silva anatarajiwa kurejea kikosi cha kwanza pembeni ya Marquinhos katika beki ya kati. Nahodha huyo wa PSG alipumzishwa kwenye mechi waliyoshinda dhidi ya Bordeaux Ijumaa.Emery atawakosa wachezaji muhimu dhidi ya Barcelona. Thiago Mota anatumikia adhabu wakati Javier Pastore anauguza majeraha.
Marco Verratti amekuwa majeruhi lakini anatarajiwa kuwa fiti kwa mechi hii.
Andres Iniesta na Sergio Busquets wanatarajiwa kuwepo tena dimbani baada ya kusumbuliwa na majeraha ya misuli.
Aleix Vidal aliyepata majeraha wikiendi iliyopita nafasi yake itatwaliwa na Sergi Roberto kama beki wa kulia.
Vikosi pamoja na mifumo yao
Paris Saint-Germain (4-3-3): Kevin Trapp; Maxwell, Presnel Kimpembe, Marquinhos, Serge Aurier; Blaise Matuidi, Adrien Rabiot, Marco Verratti; Julian Draxler, Edinson Cavani, Lucas.Barcelona (4-3-3): Marc-André Ter Stegen; Jordi Alba, Samuel Umtiti, Gerard Piqué, Sergi Roberto; Andres Iniesta, Sergio Busquets, Ivan Rakitić; Neymar, Luis Suárez, Lionel Messi.
No comments:
Post a Comment