Home » » Kikosi cha Wiki Ligi Kuu Bara
Kikosi cha Wiki Ligi Kuu Bara
Laudit Mavugo wa Simba ndiye amekuwa gumzo zaidi katika mijadala mbalimbali baada ya kufunga mabao katika mechi mbili mfululizo
Simba wamerudi kileleni baada ya ushindi wa goli 3 kwa bila dhidi ya Prisons huku hali bado siyo salama kwa klabu za JKT Ruvu, Majimaji, Toto na Ndanda wakiendelea kupigana vikumbo kwenye kushuka daraja.
Tunakuletea timu ya wiki baada ya mechi za 22 za Ligi Kuu
1.Aishi Manula- Azam
Mlinda mlango wa timu ya taifa na Azam, Manula aliinusuru klabu yake kuepukana na kichapo baada ya kuokoa michomo miwili iliyokuwa ikielekea nyavuni kwake hasa komboro la Jabir Aziz
2.Javier Bukungu-Simba
Mlinzi wa Simba raia wa Congo, Bukungu alikuwa bora Jumamosi dhidi ya Prisons ya Mbeya, alisaidia timu kwenye mashambulizi na ndiye alitengeneza goli la kwanza kutokana na krosi safi aliyoipiga
3.Mohamed Hussein-Simba
Alitimiza majukumu yake ipasavyo ya kukaba pindi wakiwa hawana mpira na kushambulia wakati timu ikiwa na mpira, mlinzi huyu anazidi kuwa bora siku hadi siku
4.Hassan Isihaka-African Lyon
Mlinzi wa zamani wa Simba, nyota huyu licha ya kucheza eneo la ulinzi lakini alifanikiwa kufunga magoli mawili kwenye mchezo uliomalizika kwa magoli mawili kwa mawili na Mtibwa
5.Aggrey Morris-Azam
Amefanikiwa kutoruhusu goli na Ruvu Shooting, Morris alifanikiwa kuwa mwiba kwa washambuliaji wa maafande hao kwa kutowapa nafasi licha ya mazingira mabovu ya uwanja
6.Jabir Aziz 'Stima'-Ruvu Shooting
Licha ya kupangiwa viungo wengi na Azam lakini kiungo huyu wa ulinzi aliweza kuwamudu vizuri na kuwazuia wasipate nafasi ya kuleta madhara
7.Raphael Alpha-Mbeya City
Licha ya klabu yake ya Mbeya City kupoteza na Mwadui ila kinda Raphael Alpha alikuwa kwenye kiwango cha juu, alitengeneza nafasi nyingi pia alifanikiwa kufunga magoli mawili kwenye mchezo huo
8.Said Ndemla-Simba
Alitawala eneo la kati dhidi ya Prisons uwanja wa Taifa, uwezo mkubwa wa kumiliki, kupiga pasi sahihi ndiyo silaha ya ushindi Simba wikendi iliyopita
9.Laudit Mavugo-Simba
Taratibu ameanza kuzoea mazingira ya hapa nchini, alitoa pasi moja ya goli na kabla na yeye kufunga moja kwenye ushindi wa goli 3 kwa bila
10.Ibrahim Ajib-Simba
Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili, Ajib hajawahi kuwa kwenye fomu nzuri kama wikendi iliyopita na maafande wa Prisons, alifunga goli moja na kutengeneza lingine kwa pasi murua.
11.Hassan Kabunda-Mwadui Fc
Ndiye aliyepeleka kilio kwenye klabu ya Mbeya City baada ya kuwatungua magoli mawili peke yake kwenye ushindi wa goli 3 kwa 2
Thanks for reading Kikosi cha Wiki Ligi Kuu Bara
No comments:
Post a Comment