Said Ndemla mwenye mpira na Simoni Serunkumu anayeruka juu
Uongozi wa Simba umegoma kumruhusu mchezaji huyo, kwa madai unamuhitaji katika kipindi hiki ambacho timu yao inapigania ubingwa wa Ligi Kuu
Kiungo mshambuluaji wa Simba Said Ndemla, amesema  ataendelea kuiwaza nafasi  aliyoipata ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kwenye klabu ya AFC Eskilstuna ya nchini Sweden.
Ndemla alisema kuwa nafasi hiyo ilikuwa ya muhimu kwake kutokana na ndoto alizokuwa nazo za kucheza soka la kimataifa kwa muda mrefu.
“Inaumiza lakini hakuna namna zaidi ya kukubaliana na maamuzi ya uongozi  kwa sababu bado ninamkataba nao, lakini imeniumiza kukosa nafasi hiyo ambayo ingeweza kuniondoa hapa nilipo na kunisogeza mbele kwenye soka la ushindani,” amesema Ndemla.
Aidha kiungo huyo, alisema baada ya kuikosa nafasi hiyo ataendelea kucheza kwa kujituma akiwa na Simba ili kuzishawishi timu nyingine kumuhitaji kwa ajili ya kumsajili kama ilivyokuwa AFC Eskilstuna, ambayo ilivutiwa naye.
Amesema hatokata tamaa kwa sababu yeye ni mpambanaji, ataendelea kucheza kwa moyo moja na kwa kiwango alichokuwa nacho anaamini ataweza kuzivutia timu nyingine na kumpa ofa nono ya zaidi hiyo ya Sweden.
Ndemla  ameibukia timu ya vijana wa Simba, kabla ya kupandishwa kikosi cha wakubwa na amekuwa akionyesha kiwango cha hali ya juu ingawa tatizo kubwa kwake ni kukosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Joseph Omog.
Uongozi wa Simba umegoma kumruhusu mchezaji huyo, kwa madai unamuhitaji katika kipindi hiki ambacho timu yao inapigania ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.